Friday, October 12, 2012

NIVYEMA KUSAMEHE NA KUSAHAU

Nakumbuka ilikuwa mwaka 1995 nikiwa darasa la tano katika shule ya msingi Nyamanoro Mwanza. Nikiwa tayari nimeshapata kipaimara toka kwa Baba Askofu John Changae, nilikuwa nimeiva kikwelikweli katika hali ya kumpenda na kutaka kumjua Mungu. Niliaminika sana kanisani japo nilikuwa na umri mdogo lakini nilipewa jukumu la kuendesha Sunday school pindi mwalimu wetu Ngere anapo kuwa anaudhuru. Kwakweli nilipenda sana kusali na kujisomea Biblia na pia nilijitahidi niwe na tabia njema isiyo mkwaza mtu wa jamii ya kistaarabu. 
Mwaka huohuo nilishikwa na butwaa kubwa ambayo ilinishangaza sana na nilibaki kinywa wazi kwani sikutegemea kama jambo la vile laweza tokea. Ilikuwa ni siku ya Jumapili ambapo Baba Askofu Changae alifika kwaajili ya kumsimika Mchungaji Noa ili awe akihudumu katika kanisa la Nyamanoro Anglican. Chaajabu kilichotokea nikwamba baadhi ya watu pale walikuwa na upupu, walianza fujo wakapakaa upupu kanisa zima, Mchungaji Kipili alianguka na kuvuja damu nyingi pale chini. Fimbo ya Askofu ilivunjwa na kutumika kama silaha ya kuadhibia. Ilisikitisha sana hali ile, waumini walitawanyika huku upupu ukiwa unawawasha katika miili yao, ngumi na mateke yalirushwa utadhania ni vita ya kikomandoo, ilitisha sana. Bahati nzuri gari la Jeshi lilipita jirani na maeneo yale ndipo msaada ulipatikana na Askofu aliokolewa na kuwa katika mikono salama ya wanajeshi.
Nilijiuliza sana kwanini hali ile itokee? Binadamu twastahili kuhukumiana kivile? Wakristo twastahili kufanya yale? Niliogopa sana na kuchukia kwenda kanisani kwani niliona ambao wanatakiwa kuwa mfano wa kuigwa wamepotea, nani ataongoza kundi iwapo hali hii imetokea? Ila nashukuru Mungu baadae nilipofika elimu ya Secondari nikamwona Baba Askofu Changae akitoa huduma katika kanisa la Nyamanoro Anglican. Nilivutiwa sana na hali ile nikaamini kuwa binadadamu tunatakiwa kusamehe na kusahau.

"Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwana neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu.Lakini kama ninyi hamsamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu" (Marko 11:25,26)
            Yesu Kristo aliyasema maneno haya kwa wanafunzi wake wa kwanza, alipokuwa akiwafundisha juu ya imani. Maneno haya ya Yesu Kristo, yanatuhusu hata sisi tulio wanafunzi wake siku hizi.Yesu Kristo katika maneno haya anazungumza na mwanafunzi wake aliyekosewa na mtu mwingine.Na katika somo hili, toka mwanzo tumechukua mtazamo huu wa Yesu Kristo; tunazungumza na mtu aliyekosewa na mtu mwingine.Somo hili lina maneno yenye mafundisho kwa mtu ambaye amekwazwa na mwenzake;mtu aliyefanyiwa kosa lolote lile.Kuna watu wengi sana wanaokosewa na watu wengine. Na tunaamini hata wewe kuna wakati fulani katika maisha yako umekwazwa na mtu mwingine.Katika ndoa makwazo yamekuwa kitu cha kawaida. Maofisini watu wanakosana kila siku. Hata na katikati ya watu wa Mungu, makwazo yanatokea mara kwa mara.Na sehemu mojawapo muhimu katika maisha ya mkristo ni maombi. Na ili tuwe na maisha ya maombi yenye mafanikio, ni lazima tuwe watu wenye tabia ya kusamehe waliotukosea.Yesu Kristo alijua jambo hili na umuhimu wa kusamehe KWANZA kabla ya kuanza kuomba.Yesu Kristo alisema, " Ninyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu".Maneno haya hayatupi uchaguzi wa kusamehe mtu wakati tunapopenda tu au wakati tunapotaka.Maneno haya ni agizo la Bwana Yesu Kristo ambalo linatakiwa lifuatwe na kila mwanafunzi wake, ili aweze kuwa na mafanikio katika maombi yake.
Haijalishi umekosewa mara ngapi, unatakiwa uwe wa msamaha. 

Imeandikwa:"Jilindeni; kama ndugu yako akikosa, mwonye;akitubu msamehe. Na kama akikukosa mara saba katika siku moja, na kurudi kwako mara saba,akisema, Nimetubu, msamehe" (Luka 17:3,4):
            Ni kweli kabisa! Mtu akikukosea na akitubu ni rahisi kumsamehe. Lakini ikiwa mtu aliyekukosea asipokuja kutubu je naye anahitaji kusamehewa?Hata asipotubu msamehe.Hili ni jambo ambalo inabidi tulizungumze kwa kufuata Neno la Mungu; maana ni jambo linalowasumbua wengi.Kuna wakati fulani tulikuwa tunalijadili jambo la kusamehe na wenzetu. Mmoja kati ya wale waliokuwepo alisema hivi: "Mimi siwezi kumsamehe mtu aliyenikosea asipokuja kutubu".Inawezekana hata wewe una mawazo kama haya. Lakini nakuuliza swali hili, "Je, kuna mstari wo wote katika biblia unaosema mtu aliyekukosea asipotubu usimsamehe?".
            Sisi hatujawahi kuuona. Kama upo tunaomba utuambie.Huhitaji kuombwa msamaha ili upate kusamehe. Biblia inasema; ‘Utusamehe deni zetu, kama sisi tuwasamehevyo wadeni wetu’ Biblia haikusema ‘Utusamehe deni zetu, kama sisi tuwasamehevyo waliotuomba msamaha!Kwa hiyo tunatakiwa kuwasamehe waliotukosea hata kama hawakutuomba masamaha.Hii ni kweli. Na sasa tuone neno la Mungu linatuambia nini:
"Kisha Petro akamwendea akamwambia, Bwana,ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara saba? Yesu akamwambia, si kuambii hata mara saba,bali hata saba mara sabini" (Mathayo 18:21,22)
            Hapa hatuoni Yesu Kristo akimwambia Petro kuwa mtu ni lazima atubu ili asamehewe. Ila anamjibu kuwa "Sikuambii hata mara saba, bali saba mara sabini"Petro alifahamu ya kuwa anahitaji kusamehe hata asipoombwa msamaha. Tatizo lake lilikuwa ni asamehe mara ngapi.Kumbuka ya kuwa unayaweza mambo yote, pamoja na kusamehe bila kuombwa msamaha, katika yeye akutiaye nguvu (Wafilipi 4:13) Tena kumbuka ya kuwa ni tabia ya Mungu iliyo ndani yako (2Petro 1:3,4) inayokuwezesha kusamehe na kusahau hata kama hujaombwa msamaha.Kumbuka si wewe unayekosewa na kukwazwa, bali Kristo aliye ndani yako. Kwa kuwa ulipompokea Kristo katika moyo wako, ulifanyika kuwa kiumbe kipya. Si wewe unayeishi, bali Kristo ndani yako (Wagalatia 2:20)

            Hata Yesu Kristo alipoteswa na kusulubiwa, na kufa msalabani, aliwasamehe waliomsulubisha na akawaombea msamaha (Luka 23:34); KABLA ya kuombwa msamaha.Na ni sauti ya Yesu Kristo inayosema ndani yako ukikosewa na mtu; "Msamehe kwa kuwa hajui alitendalo". Na Yesu akisema msamehe mtu, basi huna budi kusamehe.Na kumbuka unatakiwa kusamehe KWA AJILI YAKO MWENYEWE, hata kama hujaombwa msamaha ili na wewe usamehewe na Mungu. Usiposamehe unazuia maombi yako yasijibiwe na unazuia baraka zako nyingine.



2 comments:

  1. Ubarikiriwe kaka sana kwa kutuimarisha kiimani hata tuwe wafia dini ktk Yesu Kristu Mfufuka!Ubarikiwe sanaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaa!

    ReplyDelete
  2. Utu wema wako umekufanya utushirikishe chakula Kitakatifu cha Mungu (Neno lake lenye Uzima wa milele!

    ReplyDelete