Thursday, September 27, 2012

WEMA HAUOZI

''WEMA HAUOZI''

Ni siku nyingi kidogo, mwaka 1979, lakini ni tukio ambalo liliniuma sana.
Ilikuwa vigumu sana kulisahau na lilinifanya nijiulize, inakuwaje Mungu
anakuwa mkatili kiasi kile. Lakini bila shaka ilikuwa ni wakati ule wa
ufahamu mdogo. Hivi sasa ninafahamu mengi na hasa baada ya kujifunza
maarifa haya ya utambuzi.

Ilikuwa ni mwaka 1979 nikiwa nasafiri kutokea Dar es salaam kwenda Arusha.
Sijui ilikuwaje, lakini ilitokea. Tuliondoka Dar es salaam saa 12.30 jioni.
Wakati ule mabasi yalikuwa yakisafiri jioni na usiku, sio kama siku hizi.

Nilikuwa ninakwenda Arusha kwenye usaili kwa ajili ya ajira, nikiwa ndio
kwanza nimemaliza kidato cha nne. Niliajiriwa moja kwa moja serikalini,
kwani siku zile ajira zilikuwa ni za kumwaga. Hata hivyo sikuridhishwa na
kazi niliyokuwa nafanya, hivyo niliomba kazi kwenye kampuni moja kule
Arusha na niliitwa kwa usaili.

Tulifika mji unaoitwa Korogwe ambao wakati ule ulikuwa ndio mji maarufu kwa
hoteli zake katika barabara yote ya Segera hadi Moshi na Arusha. Tulipofika
Korogwe basi letu lilisimama kwa ajili ya abiria kupata chakula. Niliingia
kwenye hoteli moja ambayo nakumbuka hadi leo kwamba ilikuwa ikiitwa Bamboo.
Niliagiza chakula na kula haraka kutokana na muda mfupi wa kula uliotolewa
na wenye basi la TTBS ambalo ndilo nililosafiri nalo.

Wakati wa kulipa ndipo niliposhangaa na kuogopa. Niliingiza mkono mifukoni
na kukuta kwamba sikuwa na hela. Nilianza kubabaika na mwenye hoteli
alisema hawezi kukubali ujinga huo, "Abiria wengine wahuni bwana, anakula
na kujifanya kaibiwa, ukikubaliana nao kila siku hasara tu" Mwenye hoteli
alisema kwa kudhamiria hasa.

Kulizuka zogo kubwa, huku mwenye hoteli akisema ni lazima anipeleke polisi.
Ni kweli alimtuma mmoja wa watumishi wake kwenda kituo cha polisi ili
nishughulikiwe.

Hapo Hotelini kulikuwa na bwana mmoja aliyekuwa amekaa pembeni na mkewe na
watoto wao wakila. Yule bwana alipoona vile alimtuma mhudumu mmoja aniite.
Niliondoka pale kaunta nilipokuwa nabembeleza na kuja kwa yule bwana.

Alikuwa ni kijana mtu mzima kidogo, mwenye miaka kama 50 hivi. Nilimsalimia
na aliitikia, nilimsalimia mkewe pia. Yule bwana aliniuliza kisa cha vurugu
ile na nilimsimulia. Aliniuliza sasa huko Arusha ningeishi vipi wakati wa
usaili wakati nimeibiwa fedha zote na ningerudi vipi Dar. Nilimwambia
nilikuwa napanga namna ya kurudi Dar, kama huko polisi ningeaminika.

Kama mzaha vile yule bwana aliniambia kuwa angenipa fedha za kutumia huko
Arusha na nikirudi Dar nimrudishie fedha zake. Nakumbuka alinipa shilingi
90 kwa ahadi kwamba nikirudi Dar nimpelekee fedha zake ofisini kwake.
Alinielekeza ofisini kwake, mtaa wa Nkuruma na kuniambia kuwa ameamua
kunisaidia kwa sababu kila binadamu anahitaji msaada wa mwingine na maisha
haya ni mzunguko. Nilimshukuru na kuondoka kukimbilia basini. Basi lilikuwa
linanisubiri mimi tu. Nilipanda ndani ya basi na abiria wengine walinipa
pole. Tuliondoka Korogwe, lakini haikuchukua muda basi letu lilipata tatizo
la pancha ya gurudumu moja la mbele. Ilibidi tuegeshe pembeni ili
litengenezwe. Baada ya matengenezo, tuliondoka kuendelea na safari yetu.

Karibu na mji wa Same kwenye saa saba usiku, basi letu lilisimama ghafla.
Abiria walisimama ndani ya basi na kulizuka aina ya kusukumana. Huko nje
kulikuwa na ajali. Abiria tulishuka haraka na wengine huko chini
walishaanza kupiga mayowe, hasa wanawake. Niliposhuka niliona gari ndogo
nyeusi ikiwa imebondeka sana na hapo kando kulikuwa na maiti wawili.

Nilijua ni maiti kwa sababu walikuwa wamefunikwa gubigubi. Halafu kulikuwa
na katoto kalikokuwa kanalia sana kakiwa kamefungwa kanga kichwani.
Tumwahishe huyu mtoto hapo Same hospitali ameumia, ingawa sio sana.
Nilikatazama kale katoto ka kiume kenye umri wa miaka kama mitatu. alikuwa
ameumia kwenye paji la uso, lakini kalikuwa hai. Bila shaka wale walikuwa
ni wazazi wake, kalikuwa yatima tayari. Machozi yalinitoka.

Baada ya kupata msaada na askari wa usalama barabarani kuchukua maiti wale
tulipanda basini kuendelea na safari yetu. Kale katoto kalichukuliwa na
jamaa fulani waliokuwa na Land Rover ya serikali kukimbizwa hospitalini.
Ndani ya Basi mazungumzo yalikuwa ni kuhusu ajali ile tu, hadi tunafika
Arusha. Tulichelewa sana kufika Arusha kwani tulifika kwenye saa tano
asubuhi, badala ya saa mbili .

Nililala kwenye hoteli rahisi na kufanya usaili kesho yake. Ni hiyo kesho,
baada ya usaili niliponunua gazeti ambapo nilipata mshtuko mkubwa ajabu.
Kumbe wale watu wawili waliokufa kwenye ajali ile ya Same walikuwa ni yule
bwana aliyenisaidia hela na mkewe. Yule mtoto wao ndiye aliyeokoka.
Niligundua hilo baada ya kusoma jina lake na jina la kampuni aliponiambia
nimpelekee fedha zake nikirudi Dar, pamoja na picha yake, mke na mtoto.
Nililia sana, kama mtoto.

Nillishindwa kujua ni kwa nini afe. Nilijiuliza ni nani sasa angemlea mtoto
yule? Yalikuwa ni maswali yasiyo na majibu na pengine maswali ya kijinga
pia.
Nilijua kwamba nilikuwa na deni, deni la shilingi tisini. Kwa wakati ule
shilingi tisini zilikuwa ni sawa na shilingi laki moja za sasa.
Kwa mara ya kwanza sasa nilijiuliza ni kwa nini marehemu yule aliniamini
nakuamua kunipa fedha zile. Sikupata jibu.

Nilikata kipande kile cha gazeti la kingereza kilichokuwa na habari ile.
Nilichukuwa kipande hicho na kukiweka kwenye Diary yangu. Deni, Ningelipa
vipi deni la watu? Nilijikuta nikipiga magoti na kuomba mungu anipe uwezo
wa kuja kulilipa deni la mtu yule mwema kwa njia yoyote. 'Mungu naomba uje
uniwezeshe kulilipa deni la marehemu kwa sura na namna ujuavyo wewe. Nataka
kulilipa deni hili ili nami niwe nimemfanyia jambo marehemu,' niliomba.
Nilirejea Dar siku hiyo hiyo.Kwa sababu ya mambo mengi na hasa baada ya
matokeo ya usaili ule kuwa mbaya kwangu, nilijikuta nikiwa na mambo mengi
na kusahau haraka sana kuhusu mtu yule aliyenisaidia mbaye ni marehemu.
Nilifanikiwa hata hivyo kupata nafasi ya kusoma Chuo cha Saruji na baadae
chuo cha ufundi na hatimaye nilibahatika kwenda nchini Uingereza. Mwaka
1991 nilianza shughuli zangu.

Ilikuwa ni mwaka 1995 nikiwa ofisini kwangu pale lilipokuwa jengo Nasaco
ambalo liliungua mwaka 1996, ambapo lilijengwa upya na kubadilishwa jina na
kuitwa Water Front. Nikiwa nafanya kazi zangu niliambiwa na sekratari wangu
kwamba kulikuwa na kijana aliyekuwa anataka kuniona. Nilimuuliza ni kijana
gani, akasema hamjui. Nilimwambia amruhusu aingie. Kijana huyo aliingia
ofisini. Alikuwa ni kijana mdogo wa umri miaka kama 17 au 18 hivi, mweupe
mrefu kidogo. Alikuwa amevaa bora liende , yaani hovyohovyo huku afya yake
ikiwa hairidhishi sana.

Nilimkaribisha ilimradi basi tu, kwani niliona atanipotezea bure muda
wangu. Ni lazima niwe mkweli kwamba sikuwa mtu mwenye huruma sana na
nilikuwa naamini sana katika watu wenye pesa au majina. Nilimuuliza,
"nikusaidie nini kijana na ukifanya haraka nitashukuru maana nina kikao
baada ya muda mfupi". Nilisema na sikuwa na kikao chochote , lakini
nilitaka tu aondoke haraka.

"Samahani mzee, nilikuwa na shida...nimefukuzwa shule na sina tena mtu
wakunisaidia kwa sababu ...nime..niko ..kidato cha pili na hivyo tu
natafuta tu kama atatokea mtu....
Nilimkatisha. "Sikiliza kijana. Kama huna jambo lingine la kusema, ni bora
ukaniacha nifanye kazi. Hivi unafikiri kama nikiamua kumsaidia kila mtu
aliyefukuzwa shule si nitarudi kwetu kwa miguu! Nenda Wizara ya Elimu
waambie..Kwanza wazazi wako wanafanya kitu gani, kwa nini washindwe ...Kwa
nini walikupeleka shule ya kulipia kama hawana uwezo, wanataka sifa?"

"Hapana wazazi wangu walikufa na ninasoma shule ya serikali. Nimekosa
mahitaji ya msingi na nauli ya kwendea shule. Nasoma shule ya Kwiro,
Morogoro. Shangazi ndiye anayenisomesha, naye ana kansa na hivi sasa hata
kazi hafanyi..," Alianza kulia. Huruma fulani ilinijia na nilijiambia, kama
ni nauli tu na matumizi, kwa nini nisiwe mwema, angalau kwa mara moja tu.
"Baba na mama walifariki lini?" Niliuliza nikijua kwamba, watakuwa wamekufa
kwa ukimwi, maana kipindi kile ndipo fasheni ya ukimwi ilipoanza, ambapo
kila anayekufa huhesabiwa kwamba kafa kwa ukimwi.

"Walikufa kwa ajali nilipokuwa mdogo sana, nilipokuwa na miaka mitatu. Ndio
shangazi yangu akanichukua na kunilea hadi sasa anakufa kwa kansa." Yule
kijana alilia zaidi. Naomba nikwambie wewe msomaji unayesoma hapa kwamba,
kuna nguvu fulani na sasa naamini kwamba ziko nyingi ambazo huwa zinaongoza
maisha yetu bila sisi kujua.

Kitu fulani kilinipiga akilini paaa! Nilijikuta namuuliza yuel kijana. "Kwa
nini umeamua kuja kwangu, ni nani alikuelekeza hapa na wazazi wako walikufa
mwaka gani na wapi?"
Yule kijana alisema, "Nimeona nijaribu tu kwa mtu yeyote ambaye anaweza
kunisaidia, na ndio nimejikuta nikiingia hapa, sijui....sikutumwa na mtu.
Wazazi wangu walikufa mwaka 1979 huko Same na mimi wanasema nilikuwa kwenye
ajali, nikaokoka. Niliumia tu hapa." Alishika kwenye kovu juu ya paji lake
la uso.

Nilihisi kitu fulani kikipanda tumboni na kuja kifuani halafi niliona kama
vile nimebanwa na kushindwa kupumua. "Baba yako alikuwa anaitwa nani?"
"Alikuwa anaitwa Siame..Cosmas Siame.." Niliinuka ghafla hadi yule kijana
alishtuka . Nilikwenda kwenye kabati langu mle ofisini na kuchakura kwenye
droo moja na kutoka na diary. Mikono ikinitetemeka, nilitoa kipande cha
gazeti ndani ya diary hiyo, nilichokuwa nimekihifadhi.

"Ndio alikuwa anaitwa Cosmas Siame. Huyu ni mtoto wake, ni yule mtoto
aliyenusurika." Nilinong'ona. Nilijikuta nikipiga magoti na kusali. "Mungu,
wewe ni mweza na hakuna kinachokushinda. Nimeamini baba kwamba kila jema
tunalofanya ni akiba yetu ya kesho na kesho hiyo huanzia hapa duniani."
Halafu nillinyamaza na kulia sana. Nililia kwa furaha na ugunduzi wa nguvu
zinazomgusa binadamu kwa kila analofanya.

Nilisimama nikiwa nimesawajika kabisa. Nilihisi kuwa mtu mwingine kabisa.
Nilimfuata yule kijana na kumkumbatia huku nikiwa bado ninalia. "Mimi ni
baba yako mdogo, ndiye nitakyekulea sasa. Ni zamu yangu sasa kukulea hadi
mwisho" Naye alilia bila kujua sababu na alikuwa amechanganyikiwa kabisa.
Nilirudi kwenye kiti na kumsimulia kilichotokea miaka 17 iliyopita.

Tuliondoka hapo na kwenda kumwona shangazi yake Ubungo, eneo la maziwa
ambako alikuwa amepanga chumba. Kutokana na hali yake nilimhamishia kwangu,
baada ya kumsimulia kilichotokea. Huyo dada yake Cosmas alifurahi sana hadi
akashindwa kuzungumza kwa saa nzima. Alifariki hata hivyo mwaka mmoja
baadae, lakini akiwa ameridhika sana.

Kijana Siame alisoma na kumaliza Chuo Kikuu na hivi sasa yuko nchini
Australia anakofanya kazi. Ukweli ni kwamba ni mwanangu kabisa sasa.
Naamini huko waliko Mbinguni wazazi wake wanafurahia kile walichokipanda
miaka mingi sana nyuma. Lakini nami najiuliza bado. Ilikuwaje Cosmas
akanipa msaada ule? Halafu najiuliza ni kitu gani kilimvuta mwanae Siame
hadi ofisini kwangu akizipita ofisi nyingine zote? Nataka nikuambie, usiwe
mbishi sana bila sababu, kuna nguvu za ziada zinazoongoza matokeo maishani
mwetu....NGUVU HIZO NI UPENDO WA MUNGU! "

No comments:

Post a Comment