Friday, November 2, 2012

Luka 15



1  Basi watoza ushuru wote na wenye dhambi walikuwa wakimkaribia wamsikilize.
2  Mafarisayo na waandishi wakanung'unika, wakisema, Mtu huyu huwakaribisha wenye dhambi, tena hula nao.
3  Akawaambia mfano huu, akisema,
4  Ni nani kwenu, mwenye kondoo mia, akipotewa na mmojawapo, asiyewaacha wale tisini na kenda nyikani, aende akamtafute yule aliyepotea hata amwone?
5  Naye akiisha kumwona, humweka mabegani pake akifurahi.
6  Na afikapo nyumbani kwake, huwaita rafiki zake na jirani zake, akawaambia, Furahini pamoja nami, kwa kuwa nimekwisha kumpata kondoo wangu aliyepotea.
7  Nawaambia, Vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya kutubu.
8  Au kuna mwanamke gani mwenye shilingi kumi, akipotewa na moja, asiyewasha taa na kufagia nyumba, na kutafuta kwa bidii hata aione?
9  Na akiisha kuiona, huwaita rafiki zake na jirani zake, akawaambia, Furahini pamoja nami, kwa kuwa nimeipata tena shilingi ile iliyonipotea.
10  Nawaambia, Vivyo hivyo kuna furaha mbele ya malaika wa Mungu kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye.
11  Akasema, Mtu mmoja alikuwa na wana wawili;
12  yule mdogo akamwambia babaye, Baba, nipe sehemu ya mali inayoniangukia. Akawagawia vitu vyake.
13  Hata baada ya siku si nyingi, yule mdogo akakusanya vyote, akasafiri kwenda nchi ya mbali; akatapanya mali zake huko kwa maisha ya uasherati.
14  Alipokuwa amekwisha tumia vyote, njaa kuu iliingia nchi ile, yeye naye akaanza kuhitaji.
15  Akaenda akashikamana na mwenyeji mmoja wa nchi ile; naye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe.
16  Akawa akitamani kujishibisha kwa maganda waliyokula nguruwe, wala hapana mtu aliyempa kitu.
17  Alipozingatia moyoni mwake, alisema, Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa.
18  Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako;
19  sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako.
20  Akaondoka, akaenda kwa babaye. Alipokuwa angali mbali, baba yake alimwona, akamwonea huruma, akaenda mbio akamwangukia shingoni, akambusu sana.
21  Yule mwana akamwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena.
22  Lakini baba aliwaambia watumwa wake, Lileteni upesi vazi lililo bora, mkamvike; mtieni na pete kidoleni, na viatu miguuni;
23  mleteni ndama yule aliyenona mkamchinje; nasi tule na kufurahi;
24  kwa kuwa huyu mwanangu alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana. Wakaanza kushangilia.
25  Basi, yule mwanawe mkubwa alikuwako shamba na alipokuwa akija na kuikaribia nyumba, alisikia sauti ya nyimbo na machezo.
26  Akaita mtumishi mmoja, akamwuliza, Mambo haya, maana yake nini?
27  Akamwambia, Ndugu yako amekuja, na baba yako amemchinja ndama aliyenona, kwa sababu amempata tena, yu mzima.
28  Akakasirika, akakataa kuingia ndani. Basi babaye alitoka nje, akamsihi.
29  Akamjibu baba yake, akasema, Tazama, mimi nimekutumikia miaka mingapi hii, wala sijakosa amri yako wakati wo wote, lakini hujanipa mimi mwana-mbuzi, nifanye furaha na rafiki zangu;
30  lakini, alipokuja huyu mwana wako aliyekula vitu vyako pamoja na makahaba, umemchinjia yeye ndama aliyenona.
31  Akamwambia, Mwanangu, wewe u pamoja nami sikuzote, na vyote nilivyo navyo ni vyako.
32  Tena, kufanya furaha na shangwe ilipasa, kwa kuwa huyu ndugu yako alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana.

Thursday, November 1, 2012

1 Wafalme 13



1  Na tazama, akatoka mtu wa Mungu katika Yuda kwa neno la Bwana, akafika Betheli. Naye Yeroboamu alikuwa akisimama penye madhabahu, afukize uvumba.
2  Basi mtu huyo akapiga kelele juu ya madhabahu, kwa neno la Bwana akasema, Ee madhabahu, madhabahu, Bwana asema hivi, Angalia, mtoto atazaliwa katika nyumba ya Daudi, jina lake Yosia; na juu yako atawachinja makuhani wa mahali pa juu, wanaofukiza uvumba juu yako, na mifupa ya watu itateketezwa juu yako.
3  Akatoa ishara siku ile ile, akasema, Hii ndiyo ishara aliyoinena Bwana, Tazama, madhabahu itapasuka, na majivu yaliyo juu yake yatamwagika.
4  Ikawa, mfalme Yeroboamu alipoyasikia maneno ya yule mtu wa Mungu, alipopiga kelele juu ya madhabahu huko Betheli, alinyosha mkono wake pale madhabahuni, akasema, Mkamateni. Basi ule mkono wake aliounyosha ukakatika, wala hakuweza kuurudisha kwake tena.
5  Madhabahu ikapasuka, majivu ya madhabahuni yakamwagika, sawasawa na ishara aliyoitoa mtu wa Mungu kwa neno la Bwana.
6  Mfalme akajibu, akamwambia yule mtu wa Mungu, Umsihi sasa Bwana, Mungu wako, ukaniombee, ili nirudishiwe mkono wangu tena. Yule mtu wa Mungu akamwomba Bwana mkono wa mfalme ukarudishwa tena, ukawa kama ulivyokuwa kwanza.
7  Mfalme akamwambia mtu wa Mungu, Karibu nyumbani kwangu ujiburudishe, nami nitakupa thawabu.
8  Mtu wa Mungu akamwambia mfalme, Ujaponipa nusu ya nyumba yako, sitaingia pamoja nawe, wala sitakula chakula, wala sitakunywa maji mahali hapa;
9  maana ndivyo nilivyoagizwa kwa neno la Bwana, kusema, Usile chakula cho chote wala usinywe maji, wala usirudi kwa njia ile uliyoijia.
10  Basi akaenda zake kwa njia nyingine, wala hakurudi kwa njia ile aliyoijia Betheli.
11  Basi nabii mmoja mzee alikuwa akikaa katika Betheli; na wanawe wakamwendea wakamwambia kila neno alilolitenda yule mtu wa Mungu siku ile katika Betheli; na maneno aliyomwambia mfalme, hayo nayo walimwambia baba yao.
12  Baba yao akawaambia, Amekwenda zake kwa njia ipi? Kwa maana wanawe walikuwa wameiona njia ile aliyoiendea yule mtu wa Mungu aliyetoka katika Yuda.
13  Akawaambia wanawe, Nitandikieni punda. Wakamtandikia punda, naye akampanda.
14  Akamfuata mtu wa Mungu, akamkuta ameketi chini ya mwaloni, akamwambia, Je! Wewe ndiwe yule mtu wa Mungu aliyetoka katika Yuda? Akamwambia, Mimi ndiye.
15  Akamwambia, Karibu kwangu nyumbani, ule chakula.
16  Naye akamwambia, Siwezi kurudi pamoja nawe, wala kuingia pamoja nawe; wala sili chakula wala sinywi maji pamoja nawe hapa;
17  kwani nimeambiwa kwa neno la Bwana, Usile chakula wala usinywe maji huko, wala usirudi kwa njia ile uliyoijia.
18  Akamwambia, Mimi nami ni nabii kama wewe, na malaika akaniambia kwa neno la Bwana, kusema, Mrudishe pamoja nawe nyumbani kwako, ale chakula, akanywe maji. Lakini alisema uongo.
19  Basi mtu yule akarudi pamoja naye, akala chakula, akanywa maji nyumbani mwake.
20  Hata ikawa, walipokuwa wameketi mezani, neno la Bwana likamjia nabii yule aliyemrudisha;
21  akamlilia yule mtu wa Mungu aliyetoka katika Yuda, akinena, Bwana asema hivi, Kwa sababu umeiasi kauli ya Bwana, wala hukuishika amri ile aliyokuamuru Bwana, Mungu wako,
22  bali umerudi, ukala chakula ukanywa maji, hapo alipokuambia, Usile chakula, wala usinywe maji; maiti yako haitaliingia kaburi la baba zako.
23  Basi ikawa, alipokwisha kula chakula na kunywa maji, yule nabii aliyemrudisha akamtandikia punda.
24  Na alipokuwa amekwenda zake, simba alimkuta njiani, akamwua. Maiti yake ikatupwa njiani, na yule punda akasimama karibu naye; na yule simba naye akasimama karibu na maiti.
25  Na tazama, watu wakapita, wakauona mzoga umetupwa njiani, na yule simba akisimama karibu na mzoga, wakaenda, wakatoa habari katika mji ule alimokaa yule nabii mzee.
26  Na yule nabii aliyemrudisha njiani alipopata habari, akasema; Ndiye yule mtu wa Mungu, aliyeiasi kauli ya Bwana; kwa hiyo Bwana amempambanisha na simba, simba akamrarua, akamwua, sawasawa na neno la Bwana alilomwambia.
27  Akawaambia wanawe, akasema, Nitandikieni punda. Wakamtandikia.
28  Akaenda, akamwona yule maiti ametupwa njiani, na punda na simba wamesimama karibu na maiti; yule simba alikuwa hakumla maiti, wala hakumrarua punda.
29  Nabii yule akamtwaa maiti wa yule mtu wa Mungu, akamweka juu ya punda wake, akamrudisha; yule nabii mzee akaenda mjini mwake, kukaa matanga, na kumzika.
30  Akamweka maiti katika kaburi lake mwenyewe; wakamlilia, wakisema, Aa! Ndugu yangu!
31  Hata ikawa, alipokwisha kumzika, akawaambia wanawe, akasema, Nikifa mimi, nizikeni katika kaburi hili alimozikwa yule mtu wa Mungu; iwekeni mifupa yangu kando ya mifupa yake.
32  Kwa maana neno hilo alilolia juu ya madhabahu katika Betheli, kwa neno la Bwana, na juu ya nyumba zote za mahali pa juu zilizo katika miji ya Samaria, hakika litatimizwa.
33  Baada ya hayo Yeroboamu hakuiacha njia yake mbovu, lakini akafanya tena makuhani wa mahali pa juu, wa watu wo wote.
34  Kila aliyetaka akamfanya wakfu, ili wawepo makuhani wa mahali pa juu. Jambo hilo likawa dhambi kwa nyumba ya Yeroboamu, hata kuiharibu, na kuifuta usoni pa nchi.